Sunday, 4 September 2016

KANUNI ZA MSINGI KATIKA MASOMO YETU




KANUNI ZA MSINGI KATIKA MASOMO YETU

Hizi ni kanuni za msingi zitakazotufanya wanagroup wa Fikra kubwa (Great Thinkers)  tusome na kufaulu vizuri katika masomo yetu sisi kama wanagroup ili tuweze kufaulu kwa 90%, kanuni ni hizi hapa;

KUSOMA KWA MALENGO: Kuwa na malengo ni  jambo muhimu sana. Popote ulipo au kwa lolote unalolifanya lazima uliwekee malengo, mfano kama uko shuleni, lazima uwe na malengo kwamba nisome nini ili niwe hivi, nisome vipi ili niweze kufaulu kwa kiwango cha division I? au nisome kwa bidii ili kazi nitakayoipata iwe hivi n.k. jiulize lengo lako ni lipi? Ili uanze kulipigania liweze kutimia, kumbuka hata wachezaji mpira wawapo uwanjani kila mmoja ana lengo la kuibuka mshiindi dhidi ya mwingine. Kumbuka kupanga ni kuchagua hivyo wewe panga kufaulu na weka lengo katika ufaulu wa 90% kwa kila somo. Lengo ni muhimu saana hivyo USIPOTEZE LENGO.

 JIFUNZE KUTUNZA WAKATI (MUDA):Usipoteze wakati kwa mambo yasiyo na maana ambayo hayawezi kukusaidia katika maisha na masomo yako. Wanafunzi wangu kila wakati mkumbuke kuwa  wakati ni mali, sasa hivi unasoma (mwanafunzi) lakini baada ya miaka kadhaa mambo yako yatakuwa mengine. Usipoteze muda tazama mbali zaidi fikiri juu zaidi na jali muda wako. Hivyo ni muhimu sana kwa kila mwanagroup kuwa na saa yake mwenyewe.

USIKATE TAMAA: Kukata tamaa ni kati ya mambo yanayorudisha nyuma maendeleo yako kama mwanafunzi. Ni wazi wanadamu tunapaswa kuwa na nguvu, lolote baya linaloweza kutokea lionekane kuwa ni  jambo la kawaida, sawa na  kutokea kwa jambo zuri, kitu cha kutilia maanani ni kujifunza namna ya kuchukua tahadhari na jinsi ya kuishi baada ya kupatwa na tatizo.Hivyo ni marufuku kukata tamaa katika safari yetu ya elimu.

ACHA KUOGOPA KUCHEKWA: Unapokuwa na malengo katika maisha na kusoma hupaswi kuwa na aibu, kila mtu hapa duniani na maisha yake, hivyo ukatae woga kwani hauna thamani katika safari yako katika kufikia malengo uliyojiwekea, historia inaonesha watu wengi waliofanikiwa kabla ya kufanikiwa walichekwa lakini wao hawakujali walizidi kupamabana na hatimaye wakayafikia mafanikio waliyoyataka, watu wengi waliofanikiwa walichekwa na pengine kuambiwa wamechanganyikiwa ama wanapoteza muda.

PANGA KUFIKIA MALENGO YAKO HATUA KWA HATUA: Unapaswa kuwa na mikakati, kwamba unaanza na jambo fulani na baadaye unaishia na jingine, jiwekee malengo na ratiba ya kusoma kisha ufanye kama ulivyopanga, kumbuka kuacha ubabaishaji wa kuigiza unasoma na epuka kugairisha ratiba yako. Nunua saa itakayokuongoza na kukukumbusha kila wakati kuwa unajukumu la kufanya kwa wakati huo.kumbuka muda ni mali ukiupoteza huwezi kuupata tena. Hivyo zingatia ratiba yako kuliko kitu kingine chochote ili uweze kufaulu vizuri.tumia ratiba ya nyumbani kwa ukweli na uaminifu ili uweze kufaulu.

JIFUNZE KUWASAIDIA WENGINE UTAFANIKIWA:
Kusaidia wengine katika masomo ni jambo muhimu kwa sababu imani humfanya mtu kuwa na mafanikio zaidi, hasa pale anapowasaidia wasio na uwezo wa kimasomo na maisha kiujumla, lakini si wale wanaokataa kusoma na kufanya kazi kusudi. Unapopata muda wa kuwasaidia wenzako kwa yale wasiyoyafahamu darasani inakusaidia wewe kukumbuka zaidi na kuwa mbobevu katika mada hiyo. Hivyo saidia wenzako darasani kadri unavyoweza iwe mtaji kwako, fanya group discussion na presentation za kutosha utaona mabadiliko makubwa kwako.

ACHA WIVU: Ni ukweli usiopingika kuwa wanafunzi ambao wamekuwa na roho ya chuki, wivu au kununa hasa pale wanapoona mwenzao amekuwa akifanya vizuri darasani au jambo zuri darasani, mathalani kufaulu vizuri katika mitihani, hawajawahi kufaulu mitihani yao zaidi wengi walifeli vibaya mno. Mwanafunzi wangu acha wivu usiokuwa na faida kwako kila siku jenga shauku ya kutaka uwe kama mwenzako anayefanya vizuri darasani itakusaidia saana, lakini sio kufanyiana chuki na wivu usio kuwa na msingi katika masomo kwani hii itakufanya uzidi kushuka kitaaluma na mwisho utafeli kabisa, hivyo kushindwa kufikia lengo lako la kufaulu.

JIAMINI UNAWEZA KUFANYA MITIHANI NA UKAFAULU VIZURI: Mwanafunzi yeyote anaweza kufaulu katika somo lolote analolifanya ili mradi tu kama atakuwa na halli ya kujiamini (“self confidence”). Wanafunzi wengi wanashindwa kufanya vizuri mitihani yao ya Mwisho kwa sababu ya kutojiamini. Wapo wenye kuona kuwa baadhi ya division ni za kundi la wanafunzi Fulani wa shule Fulani na si wao. Sisi wanakikundi wa Great Thinkers (Fikra kubwa) tunaahidi tutajiamini na kufaulu mitihani yetu wote katika kiwango cha DIVISION I.

JIZUIE KATIKA MISISIMKO ILIYOKO MWILINI MWAKO KAMA HASIRA, NGONO, ULEVI NK: Nidhamu nzuri ni mtaji katika taaluma, hakuna taaluma nzuri katika nidhamu mbaya. Ikiwa kuna mtu/mwanafunzi anakukera ni bora ukajitenga naye, kama ni mazungumzo mnaweza kufanya baada ya hasira kushuka. Kama ni hisia za mapenzi, jiondoe toka katika mazingira yenye kukupa hisia hizo, jipe kazi yoyote ya kufanya au kujisomea vitabu, magazeti, kuangalia TV nk, ili kujitoa katika mawazo hayo ya hasira au mapenzi. Nidahmu nzuri ni jambo la msingi saana katika masomo yako, ili ufaulu ni lazima uwe na nidhamu ya hali ya juu sana kwa kila mtu, kuanzia wazazi, walimu na wanafunzi wenzako.

TAMKA MANENO YENYE MAFANIKIO SIYO YENYE MASHAKA AU KUONYESHA HALI YA KUSHINDWA, KUKATISHA TAMAA: Mfano Aaah BIOLOGY ni ngumu sana jamani, Hesabu ni ugonjwa wa taifa.Kuna watu wamezoea kusema kwa mfano Aaah mimi sijui kama nitafaulu jamani, hata mama anajua nikisoma sielewi. Aaah mimi sijui kwa nini Mungu aliniweka hapa duniani, maisha yangu ni tabu tupu, mimi nikisoma sielewi bwana nitaweza wapi kupata Division I? Epuka maneno ya namna hiyo kwani sio mazuri.

Ni hayo tu, nawatakia masomo mema kila mwenye sikio na asikie lile ambalo mwalimu analiambia kundi la Great Thinkers.
                         

















JAPHET E. MOSHI
MWALIMU MLEZI WA KUNDI( great Thinkers)

     Kwa mawasiliano zaidi ; 
                                                                                   +255 714 781 432.
                                                                                   +255 755 558 159
     E-mail address :                                             jeffmoshi@outlook.com

No comments:

Post a Comment